Buriani Rais Magufuli.

Nimetamani niandike, daftari zimalizike, na wino wangu ukauke.
Kwa moyo mzito, natafuta maneno, lakini kifo ni kizito, hakuna kauli mwafaka, ya kukieleza .
Mauko ni kama mwizi, huchukua tukipendacho.

Baba, mjomba, babu, kaka, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa awamu ya tano, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ama Kama tulivyopenda kukuita Mjomba Magu, tumepokea habari za tanzia kwa mshtuko, bado tunalia kwa sikitiko.

Kwa majonzi Alhamisi tarehe kumi na nane Machi elfu mbili na ishirini na moja alfajiri, habari ziliniatua moyo mno, ulifariki usiku wa tarehe kumi na Saba, nikatamani nisifanye kitu chochote, nikae chini nilie na kuomboleza, kumpoteza kiongozi wa kweli,kiongozi mwenye misimamo asietetereka, Shujaa wa Afrika.

Majonzi yalipokuwa yametanda, na milizamu ya machozi ilipokuwa ikichirizika , na kamasi nyembamba ziliponitoka, nikakumbukia maneno yako:  ‘Tumtangulize Mungu siku zote’.
Na kauli mbiu; ‘Hapa Kazi Tu.’

Nikafuta machozi na kupiga pua, nikakoga maji baridi na kujipa moyo. Nifanye michakato nikimbilie kwenye ujenzi wa taifa, Jembe umetuacha mkono, hakuna wa kuziba lako pengo. Falsafa zako tutazienzi milele, hukutushajiisha tuwe wavivu, bali tujipiganie kama waafrika nasi tufike kilele.

Tanzania yote tunaomboleza, Afrika mashariki , Bara la Afrika na dunia nzima kwa ujumla tumempoteza kiongozi shupavu.
Kazi zako zote na miradi uliyohakikisha imesimama itabaki kama kumbukumbu yako milele. Katu hatutakusahau, tutakuenzi mpaka siku ya Kiyama.

Wafisadi ulikuwa umewasimamisha damu, ufisadi ukapambana nao, na kuufanya haramu. Kasumba za mwenye nacho kupora mali ya umma na kuachwa huru ukazifanyia mageuzi, ufisadi ukaupiga kufuli, wote wakanyooka katika idara za umma. Mali za wafisadi zikataifishwa na mahakamani wakafikishwa.

Yote kuitetea Tanzania iwe Bora, wamachinga ukawapa vibali vya kufanya biashara zao mijini, wasihangaishwe wanapotafuta riziki.
Wanyonge ukawahurumia, elimu ya bure kuanzia chekechea hadi shule ya upili ukaianzisha, palipo kuwa na dhuluma , wanyonge ukawatetea haki waipate, tukakuita Rais wa wanyonge.

Ndege Bombardier ukatununulia, Upanuzi wa Terminal 3 uwanja wa ndege Dar-es-Salaam ukatufanyia, S.G.R ukatuletea, Stendi mpya mbezi Louis ukatujengea, Ubungo interchange ukatujengea na fly over Dar zikabobea, ukatupunguzia msongamano wa magari na vyombo vingine vya Moto, Stylers Gauge; Mradi mkubwa wa Umeme wa Julius Nyerere ukatufanikishia, Mfumo wa  uchukuzi ukaukweza, barabara na madaraja kwa wingi ukatujengea. Dar tukasema imekuwa ulaya, umeme hadi vijijini na uchumi wa saa ishirini na nne. Mwaka elfu mbili na ishirini, Tanzania ikaorodheshwa kama nchi iliyoingia kwenye uchumi wa Kati.

‘Tanzania ya viwanda’ kama ilivyokuwa kauli mbiu ya awamu ya tano, ukaifanikisha , kadri Mola livyokuwezesha. Sekta ya madini ukaisimamia, wawekezaji wasipate kurubuni uchumi, walipie ushuru, na pia wachimba madini wazawa, wakapata vibali na idhini ya riziki kujitafutia.

Maradhi ya Corona Mola alitulinda , ukasema tushikilie maombi huenda tukapata salama
‘Lockdown’ ukaipinga, kutufanyia ahueni wanyonge, ulifahamu umasikini wetu, na njaa ingekuwa janga kubwa kuliko corona.
Mola litupa tahafifu mwaka ishirini ishirini tukaumaliza pamoja.
Umeondoka Rais wetu tutakuenzi siku zote.

Mola akupokee na akueke peponi palipo na wema, umeondoka duniani Ila athari yako imebaki nyoyoni. Umetufunza mengi, mapenzi ya kweli ni kujitolea kwa ajili ya watu wengine. Ulitoa sadaka maisha yako, kwa ajili ya watanzania na Tanzania.
Kazi ya Mungu haina makosa, hakika sisi ni wa MwenyeziMungu na kwake tutarejea, kifo ni haki, na kila mmoja wetu atayaonja mauti.

Pumzika salama Dkt. John Pombe Joseph Magufuli,  Msomi wa kemia, kwa hakika dunia umeitibia, japo hukutuchoma sindano, tulikuita daktari Magufuli ,shahada ya uzamifu ulipojipatia, Tulijivunia Sana uwepo wako,ulikuwa zawadi kwetu iliyotoka kwa Mungu, athari yako itabaki milele.

*Shairi* – Buriani 
Magufuli.
Malenga -Omar Abdhallah Kimwaga.
Lakabu – *Malenga wa Dunia na Akhera.*
*Malenga Wa Diani.*

Published by omarfadhil

Motivational writer. Islam Religion Enthusiast. Coast life Writer.

Leave a comment

Design a site like this with WordPress.com
Get started