Kweli , thamani ya mwanadamu iko kwenye utu na wala sio vitu. Lakini iweje mwanadamu aishi kama hayani? Puh! Ama niseme hayawani pia ana ubora fulani, haiyumkiniki lakini ndivyo maisha yalivyo sasa hivi. Ukitaka kuleta usawa ama uungwana katika hii dunia ya sasa, utaonekana mshamba aliyeishi karne za jiwe kabla ya uvumbuzi wa chuma. Masikitiko makubwa kwamba, yasiyopendeza na kuwa kinyume yamekuwa kawaida, si wakubwa wala wadogo , wote wameangamia.
Utovu wa nidhamu na ufuska umetawala. Leo kuvaa na kutembea nusu uchi ni kawaida, eti wanasingizia ni fasheni, mitindo inayokwenda na wakati wanasema. Heri ya wale wanaomkumbuka Mungu na kutuasa kwamba tunaishi katika nyakati za mwisho, si kitambo, jamvi la dunia litakunjwa na mwenyewe Manani. Na kwa jinsi hali zilivyo, wanasema alama za awali za kiyama ama kuondoka duniani zimedhihiri.
Hivi ni mwanadamu gani mwenye akili razini , anapiga picha uchi wa mnyama na kuzianika mtandaoni, ukiulizwa utaambiwa ni modo (Model), socialite ama Mwanafasheni, Mimi hupita humo katika mitandao ya kijamii , si Facebook, Instagram, YouTube na Mingine mingi, mda mwingine macho yanajikodoa nusura yatoke .
Stara imekosekana, vilevile nisifahamike kimakosa, mitandao ina faida zake lukuki tu, lakini yuko wapi wa kuwaeleza watu wajitenge na mambo ya kipuuzi yasiyoweza kuwanufaisha kwa lolote? Watoto wanapewa simu na iwapo sio chini ya uangalizi wanapata fursa ya kuona picha hizo chafu zisizoridhisha, au hata kanda za ngono zilizorekodiwa mitandaoni, ndio kila kukicha walimu wanafunza na kuwaelekeza lakini yanaangia na upande mmoja wa sikio na kutokea sikio jingine, watashika saa ngapi iwapo vichwa vimejaa mambo yasiyo na msingi. Wasanii haswa waimbaji wa nyimbo za kizazi kipya wanakaidi kanuni za sanaa, Sanaa ni njia mojawapo ya wanajamii kueleza hisia zao na kutoa dukuduku Lao, kama katika ushairi, uandishi na tungo nyingine mbali mbali.
Ni kweli msanii haandiki kutoka nafasi hewani, ila mawazo yake yote ni athari ya mazingira yanayomzunguka, matukio aliyopitia na muingiliano wake na jamii kwa ujumla. Hii ndio sababu msanii akaitwa kioo cha jamii. Nyimbo za zamani zilikuwa na mvuto na maneno yenye hekima nyingi na yenye kuelimisha jamii, Leo mziki wa kizazi kipya kando na ule wa dini, umejawa na uchafu mwingi, video za muziki zinazoenyesha Dada zetu wakicheza nusu uchi , na maneno ya Kubomoa maadili ya jamii, yenye kuwashajiisha vijana, katika uzinzi, ubakaji, na matumizi ya dawa za kulevya.
Tumeelezwa Mara si moja kwamba , vijana ndio nguvukazi na uti wa mgongo wa maendeleo ya taifa, Leo vijana wengi hawana mwelekeo wanawaiga waimbaji kwani ndio walio na ushawishi mkubwa katika jamii , lakini je! Ushawishi huo unawapeleka wapi? Kwenye manufaa au kwenye kukosekewa. Sanaa hasa uimbaji imekuwa sehemu ya kipato kwa vijana na kuwatoa wengine katika Lindi la umaskini, na kuwasaidia wasiojiweza katika miradi tofauti, lakini ni bora kwa wasanii wetu kujikita katika tungo zinazokuwa maadili katika jamii. Niliambiwa kua uje uyaone, nikafikiri ni maembe, kumbe ni haya maisha ; Baba na mwanae wa kike wa miaka kumi na mitano washiriki ngono na kurusha kanda ya tukio Hilo mitandaoni, Mtoto wa miaka minne abakwa, Mzazi amlawiti mwanawe kwa miaka minne na kuhukumiwa kifungo cha miaka thelathini jela. Majambazi wamvamia mfugaji na kumuua kisha kuondoka na ng’ombe zake kumi, miongoni mwa habari zinazopenya maskioni kupitia vyombo ya habari, mambo mazito yasiyoleta furaha yoyote.
Mapenzi ya mali yametufikisha pabaya, watu wanaingia katika makundi ya kishetani ili nao wapate utajiri, kinachofuata ni kuwatoa kafara wazazi, ndugu , watoto, kutoa kizazi, kugeuzwa wanawake na kufanya kila linalomchukiza Mungu kwa ajili tu ya kupata mali. Wengine wanawaingilia na kuwaharibu watoto wa kiume kwa Imani ya kupata mali ili wafaulu. Wewe mwanamke uliyeolewa mbona hujawa na staha ukatulia katika ndoa yako? Vijana mke wa mtu ni Sumu, usidhihaki kwamba utakunywa maziwa, usijione kidume kuvuna alipowekeza mwenzio, utaambulia hasara kubwa. Kisha cha kusikitisha kimetokea majuzi, baada ya kijana kutembea na mke wa mtu kwa Mara kadhaa, aligunduliwa na kisha kutendewa uchafu na wanaume sita kwa kumtia adhabu juu ya kumchezea mke wa mtu, dunia ilipofika, naona isimame nishuke, Safari imenichosha na kunichusha , mbele hakutamaniki na nyuma hakurudiki , matukio ya kutisha yako njenje, ni bora kumrudia Mungu na kumtaka msamaha na muongozo, pasi na kushikilia janjajanja na kukithiri makosani.
