Mnyonge Mnyongeni.

Nyie madhalimu, mnapopanga kuhujumu na kuzima ndoto zilizoshamiri katika vifua vya watu, mnabaki kucheka na kuona poa tu. Yenu yawaendea, wenzenu wakosekewa. Kwenu ni kama kubonyeza kitufe kwenye rimoti, kubadilisha chaneli moja kwenda nyingine katika runinga, hongereni.

Hivi hamjasikia, Mungu anasema hadhulumu, na ameiharamisha dhulma baina yetu insani? Ama mmesahau Kuna na siku ya malipo? Kwa Mungu hakuna majungu, mi nna Mungu. Niseme nitawashtaki nikatafute haki, naanzia wapi mie mtoto wa masikini, msikitu ? Haki imo mikononi mwenu, Sheria mnazibadili mtakavyo. Nguvu Sina, uwezo wa kuwapiku nautoa wapi?


Kimbilio langu ni Mungu. Nikisali nitaomba Dua, Tahajjud nitasimama na kulia, kwenye sijda sitaacha kujiombea. Mungu halali, Mungu wetu sote, atajibu , haikumpendeza abadani kunifanya mimi dhalili. “Nenda uendako, fanya ufanyalo.” Ndio kauli mzinenazo, kiburi kilichoshamiri kikakita mizizi, taji la Mungu mmelivaa nyie. Mnajiona hata riziki mnaweza mkaigawa nyie.

Walimbukeni wa umaarufu, na wavivu wa kufikiri. Mgawa riziki ni Mungu, na humpa amtakaye. Hizi mnazoshikilia nyie, na juhudi tuzifanyazo chini yenu, ni sababu tu za Muumba kutufikishia hio riziki. Kusimamisha kwenu sababu, hakujamaanisha ndio mwisho wa riziki toka kwa Muumba.

Mfahamu, mnatoa nafasi ya Mungu kukunjua mipango mingine katika maisha ya mja wake. Madhalimu mtakuwa nyie mumshinde Nani? Wamepita vigogo, firauni wa Misri aliyejiita Mungu, na wababe wengine wa karne mlizosoma katika vitabu vya historia, wapo wapi leo?

Hawako katika uso wa dunia, wamefukiwa na kusahauliwa, na kwa sasa wamebaki kumbukumbu tu. Mnacheza na Mungu nyie, badilini nyoyo zenu, hakuna atakaeishi milele. Iwapo mnaona bora tukadaiane tulipane huko kwa Maulana, maana ni mbali Sana, Sina budi kusubiria, maana huko kwa Mungu ndiko kwa hakimu wa kweli.

Hakuhitajiki hata Mawakili, ushahidi wote upo, utakwendawekwa parawanja. Nimejifunza, nakwenda, kuvunjika kwa mwiko sio mwisho wa upishi. Taratibu najikongoja, matumaini hayaishi.Mgawa riziki akeli hai, Anaishi.

Mtunzi: Omar Abdhallah. Kichwa Cha Habari: Mnyonge Mnyongeni.
Makala 01:Ndoto zilizoparanganywa.

Published by omarfadhil

Motivational writer. Islam Religion Enthusiast. Coast life Writer.

Leave a comment

Design a site like this with WordPress.com
Get started